
Florence Majani, Wino Tanzania
Mara ya mwisho, miamba miwili, Paul Kagame, Rais wa Rwanda na rais wa Congo, Felix Tshisekedi, walionana kupitia mtandao wa Zoom, wakati wa mazungumzo ya kujadili mzozo wa kivita unaoendelea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. katika kikao kilichofanyika Tanzania, katika Ikulu ya Magogoni, Jijini Dar es Salaam,
Kabla ya hapo, wawili hao walitakiwa kukutana Desemba 15, kujadili mzozo huo wa mashariki mwa Congo hata hivyo hawakukutana.
Mkutano uliofanyika Tanzania chini ya wakfu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Jumuiya ya nchi za Kusini mwa Afrika(SADC) uliwakutanisha Kagame na marais wengine wa Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika na Tshisekedi yeye alihudhuria kwa njia ya Zoom. Kagame alifika Dar es Salaam, Tanzania sambamba na marais wengine, lakini katika dakika za mwisho, Tshisekedi alisema atashiriki mkutano huo kwa njia ya mtandao wa Zoom.
Marais hao wawili wameshindwa kukutana ana kwa ana kupata suluhu ya mgogoro huo ambao umesababisha maafa makubwa ya vifo, maradhi na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu DRC Congo.
Huko Doha, Tshisekedi, ambaye aliapa kukutana na Kagame “peponi tu,” amefanya mazungumzo ya amani na mwenzake Kagame baada ya miezi kadhaa ya mvutano wa kiusalama kati ya mataifa hayo mawili, wakiwa mbele ya Mfalme mwenye umri mdogo wa miaka 44 tu, mfalme wa Qatar, Sheikh Tamin Bin Hamad.

Taarifa ya serikali ya Qatar iliyotolewa jana Machi 18, imesema kuwa wakuu wa nchi hizo mbili walikubaliana juu ya umuhimu wa kuendeleza mazungumzo yaliyoanzishwa huko Doha ili kuweka msingi imara wa amani ya kudumu, kama ilivyokusudiwa katika mchakato wa Luanda/Nairobi, ambao sasa umeunganishwa na/au kupangiliwa upya.
Rais Kagame na Tshisekedi waliishukuru Serikali ya Qatar na Mtukufu Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani, Emir wa Nchi ya Qatar, kwa kuandaa mkutano huo, ambao umechangia kujenga imani katika mazungumzo yanayoendelea ya amani.

Sheikh Tamim ni nani?
Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani, alizaliwa mwaka 1980. Amepata elimu ya msingi katika shule ya Sherbone, baadaye elimu ya juu ya sekondari shule ya Harrow, na kisha akajiunga na mafunzo maalum ya kijeshi, katika chuo cha Sandhurst, Uingereza na kuhitimu mwaka 1998.
Katika shule hii ya kijeshi, ndimo walimosoma pia Mwana Mfalme, William na Harry, Watoto wa mfalme Charles 11 wa Uingereza.
Alisimikwa kuwa mfalme wa Qatar, Juni, 2013, akiwa na umri wa miaka 33 tu, akiwa ni mrithi wa baba yake, Sheikh Hamad bin Khalifa Al Thani, ambaye ameongoza taifa hilo kwa miongo miwili.
Sheikh Tamim, mbali na kuwa Mfalme, amewahi kushika nyadhifa mbalimbali, amewahi kuwa rais, wa Kamati ya Michezo ya Taifa ya Olimpiki ya Qatar, Kamanda Msaidizi Mkuu wa jeshi la Qatar, Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Kombe la Dunia, mwaka 2022.
Sheikh Tamim alitangazwa kuwa mrithi wa baba yake baada ya kaka yake mkubwa, Sheikh Jassim, kujitoa katika mamlaka ya urithi ya koo za Al-Thani.
Katika hali ambayo haikutegemewa hasa ikiwa majaribio ya kuwakutanisha Tshisekedi na Kagame yakikwama, hoja kubwa inayoibuliwa ni je Mfalme Sheikh Tamim amewezaje?
Kwa wachambuzi wa masuala ya kidiplomasia, Sheikh Tamim kuwakutanisha Kagame na Tshisekedi, si kwa kushangaza kwani katika wakati wote wa uongozi wake, kwani sera yake kuu ni kutumia nyenzo ya sera za ushirikiano na mataifa mengine, makundi katika mrengo wa siasa.
Aliingilia mzozo wa Ukraine
Juni 5 mwaka jana, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy alikutana na Mfalme Tamim ili kumshukuru kwa ushirikiamo alioutoa wa kuwarudisha Watoto wa Ukraine waliotekwa kwa nguvu na Urusi.
Urusi, imeshutumiwa kwa kuwateka maelfu ya watoto na vijana wa Kiukreni na kuwapeleka Russia tangu mwanzo wa vita mwezi Februari 2022.
Mnamo 2005, alianzisha Oryx Qatar Sports Investments, ambayo inamiliki klabu ya Paris Saint-Germain F.C. pamoja na uwekezaji mwingine. Mnamo 2006, aliongoza kamati ya maandalizi ya Michezo ya 15 ya Asia iliyofanyika Doha. Chini ya uongozi wake, nchi zote wanachama zilihudhuria tukio hilo kwa mara ya kwanza katika historia yake
Mnamo Mei 2022, Tamim alikutana na Ayatollah Ali Khamenei na Rais wa Iran, Ebrahim Raisi na kujadili suluhisho la matatizo ya nchi za kanda, ikiwemo Syria, Iraq, na Yemen.
Mzozo Wa Misri, Israel
Mnamo Novemba 2023, Qatar ilisimamia makubaliano kati ya Misri, Israel, na Hamas. Makubaliano haya, kwa ushirikiano na Marekani, yaliruhusu uokoaji salama wa raia kutoka Gaza yenye machafuko.
Mzozo Wa Urusi/Ukraine
Mnamo tarehe 13 Oktoba 2022, Tamim alikutana na Rais wa Urusi, Vladimir Putin, katika mji mkuu wa Kazakhstan, Astana. Qatar ilifanya kazi kama mpatanishi katika mazungumzo kati ya Urusi na Ukraine.
Sheikh Tamim ana wake watatu na Watoto 13
Alimuoa mke wake wa kwanza, Sheikha Jawaher Bint Hamad Al Thani, Januari 2005 na wakabarikiwa Watoto wanne
Alioa mke wake wa pili, Sheikha Al- Anoud Mana Al Hajri, March 2009, na kwa mke huyu alipata Watoto watano.
Februari 25, alimuoa mke wake wa tatu, Sheikha Noora bint Hathal Al -Dosari. Na wakabarikiwa Watoto wanne.
Kwa ujumla Sheikh Tamim Al Thani, ana Watoto 13, wanaume sana na wanawake sita kutoka katika wake zake watatu.
Utajiri wa trilioni 500 TSH
Sheikh Tamim anadhaniwa kuwa na utajiri wa takriban pauni bilioni 1.6 pekee, sawa na trilioni 500.4 za kitanzania. Familia ya Thani ina uwekezaji katika mali mbalimbali duniani, ikiwamo jumba la Shard la London, Kijiji cha Olimpiki, duka la Harrods, Canary Wharf, Chelsea Barracks na Jumba la Empire State la New York.