Takwimu za wafungwa na mahabusu Tanzania bara zilizotolewa na Ofisi Ya Taifa Ya Takwimu Tanzania, (NBS), zinaonyesha kuwa mwaka 2023, wahalifu 802 walihukumiwa kifo.
Wafungwa hao wa adhabu ya kifo waliokuwepo magerezani kati yao, 176 sawa na asilimia 21.9 rufaa zao zilikataliwa na wafungwa 626 sawa na asilimia 78.1 waliendelea kusubiri kusikilizwa kwa rufaa zao.
Wakati takwimu hizi zikionyesha hivi, ni miaka 29 sasa Tanzania haijatekeleza adhabu ya kifo kwa wafungwa waliohukumiwa kifo.
Wadau wa haki za binadamu, ikiwamo mahakama ya Afrika ya haki za binadamu na watu,(AFCPR) na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu(LHRC) wameendelea kufanya uchechemuzi wa kufanyika mabadiliko ya sheria, ya kuondoa adhabu ya kifo.
Wajawazito, wenye Watoto kifungoni
Wakati huo huo, takwimu hizo zinaonyesha kuwa, mwaka 2023, wahalifu wajawazito walikuwa 22 na wenye Watoto walikuwa 52.
Makosa yaliyoongoa kuwa na idadi kubwa ya wahalifu wajawazito na wenye Watoto ni mauaji. Asilimia 18 walihukumiwa kwa makosa ya mauaji, na asilimia 13, kujeruhi na shambulio, asilimia 10 walihukumiwa kwa wizi.