Chama cha Majaji Wanawake Tanzania (TAWJA) kimesema changamoto kubwa ambazo majaji wanawake hukutana nazo katika kutimiza majukumu yao ni wanawake kuondoa mashtaka yao dhidi ya watuhumiwa kutokana na hofu, kukosa fedha na vitisho.
Hayo yameelezwa na Mwenyekiti wa TAWJA, ambaye pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania Barke Sehel wakati wa mkutano na waandishi wa habari leo, Desemba 19.
Jaji Barke amesema wanawake wanaofungua mashtaka kwa mfano ya unyanyasaji wa kijinsia, wengi wao hushindwa kuendelea na kesi kutokana na mfumo dume kuanzia ngazi ya familia.
“Kwa mfano, mwanamke ambaye amejeruhiwa na mume wake, anaweza akaulizwa na wanafamilia, kwa hiyo mume wako akifungwa, hawa Watoto nani atawaangalia,au mume amebaka, badala kesi iendelee mwanamke anaambiwa aimalize kifamilia,” amesema Jaji Barke.
Amesema baadhi ya wanawake hulazimika kuondoa mashtaka kwa kukosa fedha za nauli wakati wa ufuatiliaji, fedha za kuendesha kesi na wakati mwingie wanaowashtaki kutumia rushwa ili kuwakandamiza.
Jaji Barke amesema hayo wakati chama hicho kikitoa taarifa ya maadhimisho ya miaka 25 ya TAWJA, yanayotarajiwa kufanyika Januari 25 mwaka 2025 mkoani Arusha, huku mgeni rasmi akitarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan.
KESI ZA ULAWITI WATOTO WA KIUME ZINASHTUA
Akitoa taswira ya mfumo wa kesi za jinai nchini, Jaji Mfawidhi Mstaafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi Sophia Wambura amesema mwenendo wa kesi za Tanzania umejawa na matukio ya kesi za ulawiti kwa Watoto wa kiume.
“Kesi za Watoto wa kiume kuingiliwa kinyume na maumbile ni nyingi sana, yaani zamani ilikuwa ni katika baadhi ya mikoa lakini siku hizi, kila mahali, kesi hizo zinakithiri, tunaona hili ni tatizo,” amesema
Jaji Mstaafu Wambura amesema kadhalika kesi za mirathi, ardhi nazo zinashika kasi katika mahakama nyingi nchini.
Hata hivyo, Jaji Barke amesema, safari ya kuongeza idadi ya wanawake katika mfumo wa sheria, inaendelea kwani kihistoria, mfumo wa mahakama ulikuwa umetawaliwa zaidi na wanaume.
“Ilishazoeleka kuwa mwanamke hawezi kushika nafasi ya juu katika ngazi ya mahakama kutokana na maumbile yake, anaonekana si mtoa maamuzi,” amesema.
Majaji hao wamezungumzia maadhimisho ya miaka 25 tangu kuanzishwa kwa TAWJA na kusema, pamoja na changamoto zilizopo lakini kumekuwa na maendelo katika ongezeko la majaji wanawake na kusema kati ya majai 36 wa mahakama za rufaa,13 ni wanawake, kati ya majaji 110 wa mahakama kuu, 34 ni wanawake na kuna msajili mmoja wa mahakama, mwanamke.
Maadhimisho ya miaka 25 ya TAWJA kwa mwaka 2025 yatafanyika mkoani Arusha na yanatarajiwa kushirikisha wadau wakiwamo, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu(LHRC), Chama cha Wanasheria Tanganyika(TLS), Chama cha Wanasheria Wanawake(TAWLA), Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania(TAMWA), na Shirika la Umoja wa Mataifa linalosimamia Wanawake(UN-Women).