Wadau wa habari wameelezwa kuwa, licha ya changamoto lukuki katika sekta ya habari, bado serikali ya Tanzania imeendelea kusajili vyombo vya habari hasa vyombo vya habari vya mtandaoni.
Akizungumza mbele ya wadau hao leo, Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amesema, jumla ya vyombo vilivyosajiliwa ni 1023 na kati ya hivyo, 355 ni vya mtandaoni.
Amesema kuna magazeti 179, majarida 174, vituo vya redio 247, vyombo vya habari vya mtandaoni 355 na televisheni, 68.
Msigwa ameyaeleza hayo leo Desemba 18 mbele ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Palamagamba Kabudi, katika mkutano uliowakutanisha wadau wa habari na Waziri huyo leo.