- Profesa Janabi atoa suluhisho
Idadi ya mbegu za kiume kwa wanaume Tanzania na duniani imepungua kwa asilimia 50 katika kipindi cha miaka 50 iliyopita.
Utafiti uliofanywa na Chuo cha Braun, cha nchini Uingereza, na kuchapishwa katika jarida la ‘Human Reproductive Update’ umebaini kuwa chanzo cha kushuka kwa idadi ya mbegu za kiume huenda kimeanzia kwa mama kwenda kwa mtoto, tangu mtoto akiwa tumboni.
Mtafiti Mkuu katika utafiti huo, Dk Hagai Levine amesema sababu za kushuka kwa idadi hiyo ni pamoja na mtindo wa maisha
“msongo wa mawazo wa mama wakati wa ujauzito, kuvuta sigara wakati wa ujauzito, matumizi ya plastiki na kemikali zilizo katika plastiki hasa kemikali za ‘phthalates’ huharibu ukuaji wa mfumo wa uzazi wa mwanaume” amesema Dk Levine katika utafiti huo.
Katika utafiti huo imeelezwa kuwa mtindo wa maisha pia huchagiza kushuka kiwango cha kuzalishwa kwa mbegu za kiume, hasa kukosa mazoezi na mlo usiofaa.
Watafiti hao walijaribu kufanya uchambuzi kwa baadhi ya miaka kuona hali ilivyo na kubaini kuwa idadi ya mbegu za kiume ilianza kupungua kwa kiwango cha asilimia 1.16 kwa mwaka, baada yam waka 1973 hadi asilimia 2.64 baada yam waka 2020.
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Profesa Mohamed Janabi, amesema idadi amesema chanzo cha kupungua kwa mbegu za kiume ni matumizi makubwa ya plastiki zenye kemikali za BPA na pyhlalates, ambazo huathiri mfumo wa vichocheo(hormones).
Profesa Janabi amesema plastiki zenye kemikali za BPA, huvuruga mfumo wa kemikali na kuharibu kiwango cha mbegu za kiume.
Chanzo kingine cha kushuka kwa idadi ya mbegu za kiume ni vyakula vyenye mafuta mengi yaliyochakatwa, sukari nyingi na vyakula vilivyosindikwa.
Sababu nyingine amesema ni kukosa muda sahihi wa kulala na msongo wa Mawazo.
NINI CHA KUFANYA
Profesa Janabi amesema ili kuondoka na tatizo la kushuka kwa idadi ya mbegu za kiume, ameshauri kula vyakula vya asili vyenye virutubisho.
“Chagua bidhaa zenye lebo inayoonyesha kuwa bidhaa haina sumu au harufu au kemikali,” amesema
Kadhalika ameshauri kuacha matumizi ya bidhaa za plastiki na badala yake kutumia zaidi glasi.
Ameshauri wanaume kula zaidi mboga za majani na vyakula vyenye mafuta ya asili kama parachichi, Samaki aina ya salmoni na karanga.
“Vyakula hivi husababisha kuongezeka kwa homoni zinazozalisha mbegu za kiume” amesema
Ameshauri wanaume kupata muda wa kulala, kupunguza msongo wa Mawazo kwa kufanya mazoezi na mazoezi ya kupumua(yoga).
Katika utafiti huo, sampuli 223 za mbegu za kiume kutoka nchi 53 duniani ikiwamo Tanzania zilifanyiwa utafiti.