Ni katika Kijiji cha Rubasazi, wilaya ya Morogoro vijijini, jua linawaka na jua linazama, lakini familia hii ina kilio kisichokwisha. Kilio hicho ni cha Yasir Nesto, mtoto wa miaka 9, ambaye furaha yake imepokwa na ugonjwa wa ajabu unaomsumbua.
Yasir, anaugua ugonjwa wa ajabu wa ngozi, ambao humsababishia maumivu makali na muwasho katika eneo la kiuno, makalio hadi mgongoni, hali inayomfanya kulia usiku na mchana.
Baba Mzazi wa Yasir, Nesto Rashid, anasema mwaka 2015 wakati Yasir anazaliwa wakunga walibaini alama ndogo nyeusi katika eneo la makalio yake lakini wakadhani ni alama tu ya kuzaliwa.
“alipoanza kukaa, ile ngozi ikaanza kumuwasha lakini kwa kuwa tunaishi maeneo ya vijijini tulikwenda hospitali za kawaida na mara zote tulipewa dawa za kutuliza maumivu,” anasema
Anasema mwaka 2018, alikuja jijini Dar es Salaam na akaelekezwa hospitali moja iliyopo Chanika, lakini baadaye akaambiwa aende hospitali ya Rufaa ya Amana. Madaktari wa ngozi katika hospitali ya Amana wakamshauri aende India.
“Madaktari wakanambia niende India, lakini hakuwapima chochote zaidi ya kutuandikia dawa za Ngozi na za maumivu” anasema
Anasema hata hivyo hali ikazidi kuwa mbaya na mtoto akaendelea kuumwa na kulia sana.
Anasema lakini kadri mtoto alivyokuwa anaendelea kukua ndivyo alama ile ikasambaa kuzunguka kiuno, mpaka mgongoni na kuwa kama uvimbe mweusi.
“Kutokana na hiyo hali, Yasir amekuwa ni mtu wa kujikuna na kulia maumivu kwa sababu lile liuvimbe limepanda mpaka mgongoni na kumfanya atembee kama kikongwe,” anasema
Baba yake Yasir anasema wamejaribu kutafuta matibabu ili kumsaidia mtoto wake bila mafanikio.
“Tulianza hapa Morogoro katika hospitali ya Wilaya lakini walichotupa ni dawa ambazo hazikusaidi chochote, wakatuambia kinachomsumbua mtoto wangu ni ugonjwa wa gozi na wakaniandikia barua niende Muhimbili,” anasema
Hata hivyo kwa mujibu wa utaratibu ilibidi waanze kwanza Hospitali ya Amana, Ilala, ambako madaktari bingwa wa gozi walifanya vipimo vya ngozi.
Walipofika Amana walipewa dawa za kutuliza maumivu na baadaye wakaambiwa waende Muhimbili wakamuone daktari bingwa wa magonjwa ya Ngozi.
“Baada ya kufika Muhimbili, madaktari walifanya uchunguzi wa awali, na wakamchoma sindano tano hapo hapo, kwa kweli zile sindano kama zilimpa nafuu kubwa, akajisikia vizuri,” anasema
Anasema madaktari waliwaambia warudi Muhimbili baada ya siku tatu kwa ajili ya vipimo zaidi.
“Tulipofika pale, tuliambiwa tulipe Tsh 700,000 kwa ajili ya vipimo, fedha ambazo hatuna,” anasema
Nestor, baba yake Yasir anasema kutokana na kazi yake ya ukulima ameshindwa kukusanya kiasi hicho cha fedha na hivyo anahitaji msaada.
“Mke wangu, Regina, kwa sasa anasumbuliwa sana na kifua kwa sababu ya kumbeba muda wote Yasir, hana msaada kifedha,” anasema
Wino Tanzania imezungumza na Daktari Bingwa wa Uchunguzi wa magonjwa, kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, kuhusu ugonjwa wa Yasir.
Dk Mwakigonja amesema Yasir anaugua ugonjwa nadra kuwapata watu(rare diseases) ambao kiini chake ni alama ya kuzaliwa(birth mark). Amesema alama ya kuzaliwa, kwa baadhi ya watu huweza kukua, kubadilika umbile, kuwasha na kuuma na kusababisha athari katika mwili, endapo haitatibiwa.
Anasema kitaalamu ugonjwa wa aina hiyo huitwa Congenital Melanocytic Naevi, ambao humpata mtu 1 kati ya 100.
“Wataalamu wa afya walitakiwa kushauri mara tu baada ya kuzaliwa, wangemshauri kufuatilia alama hiyo, na endapo ingeonyesha dalilia za kukua, kubadilika kimaumbile, kuwasha ama kuuma, ingeondolewa mapema,” anasema
Soma zaidi: https://dermnetnz.org/topics/congenital-melanocytic-naevi
Anasema kwa sasa matibabu yake yanahitaji jopo la madaktari na huenda yakawa ni gharama kubwa.
Regina Shaban, mama yake mzazi Yasir anasema: “Ninambeba kila niendako, kwa sababu ni mtu wa kulia maumivu kila wakati, na kwa sababu ngozi imejaa mpaka mgongoni, hawezi kutembea, na hiyo hali imenifanya naumwa kifua sana,” anasema na kuongeza:
“Ninaomba msaada wenu watanzania, mwanangu apone.”
Endapo familia hii itapata Tsh 700,00 za matibabu ya kuanzia, huenda familia hii ikapata ahueni ya mzigo huu wa maradhi na huenda ikamsaidia Yasir ambaye hata ndoto za kuwa na elimu zimefifia.
Unaweza kumsaidia Yasir kwa kupitia namba ya baba yake;
0782590180 AU Wino Tanzania kwa namba 0764438084