Manusura aliyeokolewa baada ya kufunikwa na kifusi katika jengo la ghorofa Kariakoo juzi, Khadija Musa, anawaomba watanzania, jeshi la polisi, na Rais, kumsaidia kupata mtoto wake, Nathan Said, ambaye amekwama ndani ya kifusi katika jengo hilo.
Khadija, amezungumza na WINO Tanzania na kusema:
“Mi naomba mwenyezi Mungu,naomba serikali yangu, nawaomba wananchi, niupate hata mwili wa mtoto wangu, mimi nimekubali, niupate mwili tu, mwili tu, mi nitaridhika, mwanangu mpaka leo hawezi kuishi na njaa,”
Khadija mkazi wa Kibada anaelezea hatua kwa hatua kabla maafa hayo hayajamkuta.
Anasema kwa kawaida, yeye huchukua bidhaa katika jengo hilo sehemu ya chini, na kupanda juu kuziuza kwa bei ya reja reja.
“Siku hiyo niliamka saa moja asubuhi, kama kawaida, na nikashuka kule chini kama kawaida, nimeshachukua bidhaa napanda juu, ghafla nikasikia kelele, mwanangu simuoni” anasema
Khadija anasema hali ilikuwa mbaya na mpaka amefanikiwa kuokolewa ni Mung utu.
“Hali ilikuwa ni ngumu, sikujua kama ntatoka, ila Mungu hakutaka mwanangu apone. Nimekaa kule kuanzia hiyo asubuhi, na jana asubuhi ndio nimejikuta nipo hospitali ya Amana” anasema
Anasema kwa kuwa hakuwa ameumia, aliruhusiwa ili kupisha idadi kubwa ya majeruhi waliokuwepo hospitali.
Khadija anasema katika tukio lile mtoto wake alitoweka palepale, lakini kwa kutumia simu za wengine waliokuwamo chini, walikuwa wanawasiliana na walio nje hadi timu ya waokoaji ikawafikia.
Jengo hilo la ghorofa lilianguka juzi Novemba 16 na mpaka sasa watu 16 wamethibitishwa kufariki dunia, huku wengine 86 wakiokolewa.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameongoza mamia ya waombolezaji leo katika viwanja vya Mnazi Mmoja kutoa salamu za mwisho za watu 16 waliopoteza maisha.
Mawasiliano ya Zainab haya hapa: 0717399189