Wino Ripota
Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimetoa taarifa rasmi kwa umma ikiwa ni hatua ya kujibu tuhuma mbalimbali ambazo zimekuwa zikielekezwa kwa chama hicho.
Katika taarifa yao iliyotolewa leo na Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema, CHADEMA kimesema, kimeamua kujibu tuhuma ambazo kwa muda mrefu zimekuwa zikielekezwa kwa chama hicho ambazo kimsingi, zimesababisha wanachama wa Chadema kutaka ufafanuzi.
Kabla ya taarifa hii, Naibu Katika Mkuu wa Chadema(Bara) Tundu Lissu, amekuwa akiibua hoja kukihusu CHADEMA, katika mikutano yake anayofanya na wanahabari.
Moja ya hoja ambayo Lissu amekuwa akiibua ni pamoja na kuwa Chama, yaani Chadema kilidanganywa kuhusu suala la maridhiano kwa kuahidiwa baadhi ya nafasi za uongozi ikiwamo ya Uwaziri Mkuu na Makamu wa Rais.
Mei mwaka huu Lissu akiwa katika Mkutano wa hadhara uliofanyika Mkoani Iringa, alisema: “Kuna mtafaruku mkubwa sana wa uchaguzi ndani ya chama chetu, kuna pesa nyingi ajabu kwenye uchaguzi huu (ndani ya CHADEMA),”
Madai ambayo yanaenda sambamba na Lissu kulalamika kuwa amekuwa akiambiwa na uongozi wa chama chake kuwa hakuna pesa za kulipia mikutano yake ya hadhara, lakini anashangaa kuona kuna pesa za rushwa kwenye uchaguzi wa ndani.
Hata hivyo taarifa ya Chadema imefafanua kuwa, chama hakijawahi kuletewa hoja ya kugawana majimbo,nafasi za Madaraka kutoka kwa serikali.
Kadhalika Chama hicho kilitoa ufafanuzi ya kuwa, nafasi ya umakamu wa Rais ni ya kugombewa na haitolewi mezani kwa mujibu wa katiba ya nchi kwa sasa.
“Katika vikao vyote CHADEMA haijwahi kutoa au kupokea mapendekezo yoyote ya serikali ya ‘nusu mkate’ jambo hili halijawahi kuwa sera ya Chadema,” imesema taarifa hiyo.
Chadema katika taarifa hiyo kimesema kimekuwa katika program za kukiuhisha chama baada ya kupitishwa kwa kile walichokiita, ‘Bonde la uvuli wa mauti’ kwa miaka saba.
Kadhalika Chadema kimejibu tuhuma za matumizi mabaya ya rasilimali fedha na rushwa ndani ya chama hicho na kusema:
“Hivyo basi tunamwalika mtu yeyote mwenye Ushahidi au vielelezo vinavyotosheleza, kuwezesha kuchukua hatua za kinidhamu kwa wahusika,awasiliane na ofisi ya katibu mkuu au ofisi ya katibu yeyote wa kanda”
Katika hitimisho lao, Chadema kimewataka wanachama wake kuwekeza zaidi katika uchaguzi wa serikali za mitaa na kupuuza propaganda za kukigawa chama.