Wino Ripota
Utafiti mpya umebaini kuwa zaidi ya watu wazima milioni 800 duniani wanaishi na ugonjwa wa kisukari, idadi mara mbili, ukilinganisha na miongo mitatu iliyopita.
Utafiti huo uliochapishwa jana na jarida la Afya la Lancet umekuja katika wakati ambapo dunia leo inaadhimisha Siku ya Kisukari.
Katika utafiti huo, madaktari wamebaini, idadi ya watu wazima wenye ugonjwa wa kisukari, imeongezeka kutoka asilimia 7 mwaka 1990 hadi kufikia asilimia 14 mwaka 2022.
Shirika la Afya Duniani,(WHO) kwa kushirikiana na Shirika la Magonjwa Yasiyoambukiza(NCD-RisC) walifanya utafiti huo wa aina yake kuangalia kiwango cha magonjwa ya kisukari duniani wakitumia takwimu za watu 140 milioni.
Watu wazima wenye umri wa kuanzia miaka 18 na zaidi walifanyiwa uchunguzi katika nchi 1000 duniani, na kubaini namna ugonjwa wa kisukari unavyoathiri watu.
Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Profesa Mohamed Janabi, ametoa dondoo za kufuata ili kumaliza kabisa ugonjwa wa kisukari aina ya pili (Type 2Diabates).
Katika ukurasa wake wa X, Janabi amesema:
“Sio lazima uishi milele na kisukari Aina ya Pili. Nini cha kufanya?
Profesa Janabi amesema ili kuondokana kabisa na ugonjwa huo, ni muhimu kufanya yafuatayo.
1. Kufanya mazoezi dakika 30 angalau mara tatu kwa wiki au hatua 10,000 kwa siku 2 kwa wiki.
2. Pata usingizi/kulala kwa kutosha kati ya saa 6 hadi 8.
3. Ongeza ulaji wa matunda na mboga za majani.
4. Punguza sana sukari.
5. Acha kabisa sukrai na vyakula vyenye sukari.
6. Jiepushe na mihemko.
Wakati huo huo, Mkurugenzi wa WHO, Dk Tedros Adhanom Ghebreyesus, amezungumzia utafiti huo wa Lancet na kuzitaka nchi wanachama kuanza kuchukua hatua dhidi ya ugonjwa huo.
“Tumeona ongezeko la kutisha la kisukari, katika miongo mitatu iliyopita, ambayo inaonyesha chanzo ni unene kupindukia, ambao kimsingi unachagizwa na madhara ya kuuzwa kiholela kwa vyakula visivyo na afya, kukosa mazoezi na hali ngumu ya Uchumi,” amesema Dk Tedros.
Kauli mbiu ya Siku ya Kisukari Duniani kwa mwaka huu ni “Vunja Vizingiti,Ondoa Pengo’ ambayo inasisitiza utashi wa kupunguza athari za ugonjwa wa kisukari na kuhakikisha kila mmoja anapata huduma sawa na nafuu za afya.