Wino Ripota
Katika kinyang’anyiro cha kutimua vumbi nchini Marekani, mgombea wa tiketi ya chama cha Republican, Donald Trump, anaelekea kuchukua ushindi.
Trump, ambaye aliwahi kuwa Rais wa 45 wa Marekani katika uchaguzi wa mwaka 2016, anachuana na Makamu wa Rais, kupitia chama cha Democratic, Kamala Harris katika mbio hizo za urais.
Dalili za ushindi wa Trump, zinaelezwa na wachambuzi kuwa, upo uwezekano wa kurudi tena Ikulu na kuwa Rais wa 47 wa taifa hilo kongwe duniani.
Trump alishind urais, mwaka 2016 akichuana na Hillary Clinton, akashindwa urais, 2020 akichuana na Joe Biden, na sasa anachuana na Kamala Harris, ambaye ni Makamu wa Rais wa nchi hiyo.
Matokeo ya awali ya kura yanaonyesha wazi kuwa, Trump anaongoza katika majimbo yenye ushawishi ambayo kimsingi huwa yanatabiri mshindi wa kiti cha Urais.
Kituo cha habari cha CBS News kimeonyesha Trump akishinda majimbo ya North Carolina, Georgia, Pennsylvania na Wisconsin – akizidi kiwango cha kura 270 kwa kura 6 na jumla ya kura 276. Kura bado zinahesabiwa katika majimbo mengine ya Michigan, Nevada na Arizona.
Katika safari yake ya kuusaka urais wa Marekani mwaka huu, Trump amekoswakoswa na mashambulio ya risasi mara mbili, kwanza akiwa katika mkutano wa kampeni eneo la Buttler, jimbo la Pennysylvania, Julai 13 na Septemba 15 eneo la Palm Beach Golf Club.
Mwezi huo huo, Trump alimchagua Seneta wa Ohio, JD Vance, kuwa mgombea mwenza wake, huku mfanyabiashara tajiri duniani, mmiliki wa kampuni ya Tesla, na mtandao wa X, Elon Musk, akiwa mshirika wa karibu wa Trump hatua kwa hatua.
Mnamo mwanzoni mwa mwenzi Agosti, Joe Biden, rais wa Marekani, alimuachia msaidizi wake, Makamu wa Rais, Kamala Harris kuwa mgombea wa urais, baada ya kugundulika kuwa na hali mbaya kiafya.
Kuanzia wakati huo, Trump akaingia katika vita ya kisiasa na Kamala. Trump amekuwa akimshutumu Kamala kwa kuwaingiza kinyume na sheria, wahamiaji haramu na akimtaja Kamala kama mwenye uwezo mdogo wa akili ‘Low IQ’.
Sera za Trump siku zote ni kuwaondoa wahamiaji haramu na kuzuia uhamiaji haramu katika taifa hilo tajiri duniani. Trump alitekeleza sera hiyo mwaka 2017 na kuyazuia baadhi ya mataifa kuingia Marekani.
Katika hotuba yake ya mwisho jimbo la Giorgia, Trump alisema:
“Baada ya yote tuliyopitia pamoja, tulisimama pamja kwa miaka minne mikubwa katika historia ya Marekani,”
“Kwa ninavyoona miaka ijayo itakuwa mizuri sana, itakuwa ya kufurahisha sana. Hali itakuwa mbaya kidogo labda mwanzoni, lakini baadaye itakuwa bora.” Trump alisema.
Kampeni za Trump zilitawaliwa na mikiki mizito, miongoni mwao ni kesi dhidi yake. Kuanzia mwaka 2023, Trump alishitakiwa zaidi ya mara nne katika kesi tofauti, ikiwamo ya kukataa kuondoka Ikulu kwa amani mara baada ya kushindwa urais, 2020. Lakini pia, kuzuia baadhi ya nyaraka za urais nyumbani kwake mara baada ya kushindwa urais, 2020.