• Yeye ndiye mkurugenzi wa halmashauri, meya
• Yeye ndiye mtunza maktaba ya kijiji, anayesimamia mgahawa wa pekee kijijini
Wino Tanzania
Ni katika jimbo la Boyd, mji wa Nebraska, maili nne kutoka mpaka wa jimbo la Dakota nchini Marekani.
Jimbo hilo la Boyd, lenye ukubwa wa mita za eneo 535, lina watu 2,000 tu, na miji mitatu. Lina watu wasiozidi 10. Lakini Kijiji cha Monowi, yupo mkazi mmoja tu, naye si mwingine ni Elsie Eiler.
Elsie (87) ni mkazi pekee katika kijiji hicho tangu mumewe, Rudy Eiler alipofariki dunia mwaka 2004. Awali, wakati mumewe akiwa hai, Kijiji cha Monowi kilikuwa na wakazi wawili.
Kwa mujibu wa Jarida la People la nchini Marekani, Elsie licha ya kuwa ni mkazi pekee wa kijiji hicho ana shughuli lukuki.
Ni Elsie anayesimamia mgahawa pekee katika kijiji hicho uitwao The Tarven, ambao wageni wanaofika hupata chakula na vinywaji na mkazi huyo amekuwa akiiendesha mwaka 1971 ikiwa ndio biashara pekee kijijini hapo.
“Ninafanya kazi katika baa hii kuanzia Jumanne hadi Jumapili, kuanzia saa 3 asubuhi na kuwepo hadi mteja wa mwisho anapomaliza kupata huduma hata kama ni usiku mwingi,” anasema Elsie.
Elsie anasema alianza kupumzika siku za Jumatatu mwaka 2011 baada ya kugundulika ana saratani ya utumbo, ambayo hata hivyo anasema haimsumbui kiasi cha kumzuia kufanya kazi.
“Mara nyingi nafanya kazi za kusimama, kwa sababu nafanya kila kitu mwenyewe, sina msaidizi, watu ninaowaona hapa ni wageni wanaokuja na kuondoka,” anasema.
Akiwa ni mkazi pekee wa Monowi, Elsie ndiye amekuwa akisaini nyaraka za Serikali zinazotumwa kutoka makao makuu ya mji zinazohusu masuala ya fedha za maji na umeme, ujenzi wa brabara.
“Yeye ndiye meya wa Monowi, ambaye tunaweza kusema hana mpinzani, ndiye katibu muhtasi, karani na ndiye anayewasilisha maombi serikali zinapohitajika leseni za tumbaku, pombe na yeye ndiye huwa mzungumzaji mkuu pindi maofisa wa Serikali wanapofika kijijini hapo,” linaeleza gazeti la The People.
Kadhalika Elsie ndiye mtunza maktaba, mwakilishi wa Serikali na msimamizi wa shughuli za maendeleo kijijini Monowi.
Utajiuliza Elsie, hana watoto? Elsie na mumewe Rudy wamejaliwa watoto wawili, wa kike na wa kiume, ambao walihamia miji mingine Marekani, baada ya kumaliza shule.
“Palikuwa na kijana mmoja hapa anaishi, lakini aliondoka baada ya nyumba yake kuungua moto,” anaeleza Elsie.
Kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya Nebraska, Monowi iliwahi kuwa na wakazi 150 mwaka 1930 lakini, ni wakati ambapo reli ya Elkhorn ilipokuwa ikijengwa.