Ripota wa Wino Tanzania Hapana shaka kuwa siku aliyozaliwa Sylviabay Kijangwa huko wilayani Lushoto mkoani Tanga, wazazi hawakufahamu kuwa mtoto huyo amebeba maono makubwa ya kimataifa. Pengine walidhani ni mtoto wa kike kama ilivyo kwa wengine, lakini kumbe Sylviabay alikuwa amebarikiwa kuwa zaidi ya hapo. Ni Sylviabay Kijangwa, ambaye Juni, 2024 alichaguliwa kuwa Mwakilishi wa Vijana katika utatuzi wa migogoro Afrika wa Umoja wa Afrika. Awali, nafasi hiyo iliwaniwa na vijana zaidi ya 2000 kutoka mataifa ya Afrika Mashariki. Anapoishika nafasi hii, Sylviabay anakwenda kuwakilisha vijana katika mpango wa kutatua migogoro barani Afrika. “Ninawakilisha vijana katika Umoja wa Afrika na jitihada za mazungumzo na upatanishi na diplomasia ya kuzuia migogoro (dialogue and mediation and preventive diplomacy),” anasema. Safari yake haikuanza kinasibu la hasha, ilianzia pale aliposhiriki kuwa mjumbe wa vijana wa kitaifa katika Baraza la Vijana la Jumuiya ya Madola (Commonwealth Youth Council), mwaka 2022 hadi 2024) Anasema kwa kuishika nafasi hii, alipata uzoefu mkubwa wa masuala mbalimbali yanayohusu vijana na jumuiya za kimataifa.
Sylviabay Kijangwa akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Umoja wa Afrika jijini Nairobi, Juni mwaka huu, mara baada ya kuchaguliwa kuwa mwakilishi wa vijana AU.
“Ndipo Juni, 2024 Umoja wa Afrika ulitangaza fursa hii adhimu ya uongozi na uwakilishi wa vijana katika jitihada zake kutatua migororo Afrika (Wise Youth). Nikaomba nafasi hii na kupitishwa kwenye hatua za mchujo na baadae kufanya usahili Umoja wa Afrika,” anasema na kuongeza: “Namshukuru Mungu nilifanikiwa kuvuka na kuteuliwa kushika nafasi hii kwa muda wa miaka mitatu nikiiwakilisha Tanzania na Umoja wa Afrika Mashariki.” Pamoja na nafasi hiyo, kadhalika Sylvia, ni mwakilishi wa Tanzania katika Jukwaa la Umoja wa Nchi 12 za Maziwa Makuu, ikiwamo Tanzania nafasi aliyoishika kuanzia mwaka 2022 mpaka sasa. Uwezo wa Sylviabay na uzoefu katika masuala ya maendeleo ya vijana, haki za kijinsia na amani, ulimuwezesha kuteuliwa mwakilishi wa vijana kutoka Tanzania, ambaye alishiriki katika mchakato wa kuhakiki itifaki ya vijana ya SADC. “Hivi karibuni pia nimepewa heshima ya kutambuliwa kama shujaa wa Vijana na Jumuiya ya Wanasheria wa Afrika Mashariki,” anasema Sylvia na kuongeza: “Nikiwa na shauku kubwa kwa maendeleo ya vijana, nimepata uzoefu katika kuongoza na kushiriki kwenye shughuli mbalimbali za maendeleo ya vijana, masuala ya mabadiliko ya tabianchi, na kuendeleza amani katika kanda ya Maziwa Makuu na Kusini mwa Afrika.”
KUHUSU Sylviabay Amezaliwa wilaya ya Lushoto Tanga Amesoma shule ya msingi Diamond Amesoma shule ya sekondari Lord Baden Amesoma kidato cha tano na sita sekondari ya Chang’ombe Amepata shahada yake ya kwanza, katika Chuo cha Mahusiano na Kimataifa cha Diplomasia
Continue Reading