Mwandishi, Wino Tanzania
Safari ya ujauzito hadi kujifungua kwa wanawake wengi huja na mambo mengi ikiwamo ushauri, elimu dunia, mila na tamaduni za aina mbalimbali.
Ni katika wilaya ya Sengerema, mkoani Mwanza, na hapa naambiwa wajawazito walio wengi, aghalabu hufungasha dawa za mitishamba, wanapokwenda kujifungua.
Ninapohoji, ni Kwa nini wanabeba dawa hizo? Naambiwa hii ni mila ya Lwikiro. Ni mila gani hii, na ina maana gani kwa mjamzito?
Lwikiro ni mila inayotekelezwa kwa baadhi ya makabila ya wakazi wa wilaya ya Sengerema, mkoani Mwanza.
Mila hiyo iliyotumika kwa miongo mingi, miongoni mwa jamii hiyo, imejipatia umaarufu baada ya kujengeka kwa Imani kuwa, mwanamke ambaye ametembea na mwanaume zaidi ya mmoja, au kwa jina jingine amechepuka basi hupata shida wakati wa kujifungua na huweza hata kufa au kupoteza mtoto.
Hivyo basi, mwanamke wa aina hiyo huitwa Lwikiro, na hulazimika kunywa aina ya dawa za mitishamba, ili asipate madhara wakati wa kujifungua.
Vifo vya uzazi nchini Tanzania kwa sasa vimepungua kutoka 556 katika kila vizazi hai 100,000 mwaka 2016 hadi vifo 104 mwaka 2023, lakini suala la vifo vya uzazi kutokana na uhaba wa dawa na vifaa tiba au kutohudhuria kliniki si hoja kwao, bali hili la kutembea na wanawake wengi ndilo kubwa zaidi kwao.
Restuta Bernad Mkunga wa Jadi, Mstaafu wilayani Sengerema, anaeleza maana ya Lwikiro.
“Lwikiro ni mwanamke mjamzito anayechanganya wanaume, sasa wale wanaume, kila mtu ana damu yake, anapofikia muda wa kujifungua, mwanamke anapata shida,” anasema Restusta.
Sikiliza makala hii hapa: https://www.instagram.com/p/C9caEQztmx4
Sophia Madirisha, mkazi mwingine wa Sengerema, anasema wakati ule mwanamke anapojifungua, wanamuuliza umetembea na wanaume wangapi wakati una mimba, na mwanamke yule huwataja idadi na kwa majina hata kama walikuwa 20.
“Anapomaliza kuwataja tu, na mtoto anatoka lakini ni baada ya kufanya dawa za kimila,” anasema Madirisha.
Mila hii ya Lwikiro, inatumika zaidi katika watu wa jamii ya Wasukuma, ambapo wajawazito hao wanapofika katika vituo vya kutolea huduma za afya aghalabu huwa wamebeba dawa za aina mbalimbali za mitishamba ambazo, wao huzitumia ili kuzuia kujifungua kwa shida.
Frederick Mugarula, Mganga Mkuu wa Halamshauri ya Wilaya ya Sengerema, anasema katika kila wanawake 10 wanaofika hospitalini hapo, watatu huwa wamebeba dawa za mitishamba.
“Katika matumizi haya ya dawa za asili au za kienyeji, nataka niwaonyeshe kuwa zimeonyesha kuwa na madhara makubwa. Kwa mama mwenyewe mzazi anaweza akapata madhara kwenye ule mfuko wa uzazi,” anasema Dk Mugarula.
Takwimu katika vituo vya afya katika wilaya hiyo, zinaonyesha kuwa, kwa mwaka 2023, wanawake waliojifungua ni 19452. Hali hii kwa mujibu wa Dk Mugarula inaonyesha kuwa idadi ya watu wanaopata ujauzito ni kubwa huku kukiwa na Imani zinazochagiza matumizi ya dawa za asili wakati wa ujauziyo.