
Wino Tanzania
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Masoud Othman Masoud, amesusia mkutano wa Jukwaa la Demokrasia Afrika, uliopangwa kufanyika jijini Luanda Angola, leo.
Masoud amesusia mkutano huo baada ya kuwekwa kizuizini katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Quatro De fevereiro wa Luanda, Angola, kuanzia jana akiwa na viongozi wengine kutoka Afrika.
Masoud ambaye ni kiongozi wa ACT-Wazalendo, amesema, baada ya kushikiliwa katika uwanja huo wa ndege kwa saa zaidi ya nane, waliachiwa saa 4 usiku na kupelekwa hotelini, hata hivyo, amesema hatahudhuria tena mkutano huo na badala yake anarejea nyumbani Tanzania.
Kupitia mtandao wa X, Masoud ameandika:
“Hata hivyo, napenda niweke wazi kwamba pamoja na kukerwa na kuchukizwa na yaliyotendwa dhidi yetu, sina kinyongo na Raia Wema wa Taifa hili jema, ambalo Tanzania tumekuwa na mahusiano mema ya kihistoria na madhubuti kwa muda mrefu. Baada ya kuzingatia tukio la Jana, nimeamua kutoshiriki katika Mkutano Muhimu nilioalikwa, wa Jukwaa la Demokrasia Afrika, na badala yake ninarejea Tanzania.”
Pamoja na Makamu huyo wa kwanza wa Rais, Zanzibar, viongozi wengine waliokumbana na kadhia hiyo ni Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, Kiongozi Mkuu wa ACT-Wazalendo Dorothy Semu. Pamoja nao walikuwepo marais wastaafu kutoka Botswana, Columbia, Waziri Mkuu mstaafu wa Lesotho na viongozi wa vyama vya siasa Tanzania kutoka ACT Wazalendo na Chadema.
Hata hivyo, Masoud amesema, wakati wote huo alikuwa ameambatana na Balozi wa Tanzania, Zambia, anayewakilisha Angola pia, Luteni JeneraLI Mathew Mkingule.
“Naamini nahitaji muda wa kufanya tafakuri ya kina na kutathmini kile kilichotendwa dhidi yetu, ambacho kilikuwa ni shambulio dhidi ya Diplomasia na Demokrasia ndani ya Afrika” ameandika Masoud
Kwa upande wake Lissu. Ameandika katika mtandao wake wa X akisema Angola ni marafiki wa Tanzania na Tanzania imekuwa pamoja na Angola tangu wakati wa harakati za kudai uhuru.
“Kitendo cha serikali ya Angola kutuzuia kuingia Angola hakielezeki wala hakikubaliki. Ni kitendo kinachodhihirisha kile ambacho wengi tulikuwa tunakihisi: kwamba serikali ya nchi hii inatawala kiimla huku ikijifanya kuwa Angola ni nchi ya kidemokrasia,” ameandika Lissu
Kwa upande wake, Kiongozi wa ACT- Dorothy Semu yeye ameandika:
“Nimerudi salama nyumbani nikijivunia nyongeza ya uzoefu wa Luanda. Hakuna kurudi nyuma!Tuhakikishe kwamba vyama makini ndani ya nchi tupo pamoja katika kudai masuala ya msingi kwa watu wetu na wana demokrasia wa Afrika tunaunganisha nguvu na mashirikiano. Aluta Continua!