
Wino Tanzania
Msaidizi wa aliyekuwa Mwenyekiti wa CHADEMA -Taifa, Freeman Mbowe, Edward Kinabo, ameweka hadharani maneno ya mwanasiasa huyo(Mbowe) aliyoyatoa mbele ya wanachama wa Chadema alfajiri ya Januari 22 mara baada ya matokeo ya uchaguzi wa Mwenyekiti kuonyesha hajashinda katika uchaguzi huo.
Kinabo aliyekuwa akiratibu katika sekta ya habari, mawasiliano na kampeni, amesema, Mbowe alitoa wosia huo kwa wanachama wa Chadema alfajiri ya Januari 22 mara baada ya matokeo ya uchaguzi wa Mwenyekiti wa chama kuonyesha kuwa Mbowe, hajashinda uchaguzi huo.
Katika waraka wake, Kinabo amesema Mbowe hali akijua hajashinda, aliwatia moto akiwaambia:
“Msije mkawaza kuacha siasa au kuacha Chama hiki eti kwasababu mimi mliyeniunga mkono nimeshindwa. Wala msitake kuususia au kujaribu kuukomoa uongozi huu uliochaguliwa kwasababu tu mimi nimeshindwa. Hapana. Msifanye hivyo.”

Kadhalika, Kinabo anamnukuu Mbowe akisema:
“Najua na ninyi mmekuwa na ndoto zenu za kisiasa kupitia chama hiki. Ni lazima maisha mengine yaendelee. Ni lazima muendelee na ndoto zenu. Endeleeni kushikamana na Chama. Endeleeni kupigania ndoto zenu katika siasa, na endelezeni ndoto ya Chama hiki ya kuwakomboa Watanzania”,
Katika waraka wake, Kinabo amesema maneno ya Mbowe yaliwagusa, na hata kufanya wengine watokwe machozi.
Kinabo amesema, imeonekana dhahiri kuwa Mbowe hana siasa za chuki na kwamba hakugombea uenyekiti kwa ajili ya maslahi binafsi bali kwa maslahi ya chama na taifa.
“Viongozi na wanasiasa wengi huonesha busara na hekima ya kimaigizo hadharani, halafu huenda kunoa upanga sirini, lakini haikuwa hivyo kwa Mhe Mbowe,” ameandika Kinabo.