
Mbivu na mbichi zitajulikana leo ndani ya CHADEMA, iwapo Mwenyekiti Freeman Mbowe atatetea kiti chake, au Makamu Mwenyekiti-Bara, Tundu Lisu, atachukua kijiti au ni Odero Charles Odero.
Mkutano Mkuu wa CHADEMA unafanyika leo ili kumpata Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti ambao wataiongoza Chadema kwa miaka mitano ijayo.
Haya yanafanyika katika siku ambayo Chadema inatimiza miaka 32 tangu kuzaliwa kwake Januari, 1993.

Uchaguzi wa leo wa Chadema unakwenda kutoa taswira ya ukomavu wa kidemokrasia ndani ya chama hicho lakini katika medani za siasa za vyama vingi nchini.
Mitandaoni, wachambuzi wa masuala ya siasa, wanaharakati kila mmoja amekuwa na maoni yake kuhusu tukio hilo.
Mwanaharakati wa masuala ya siasa na jinsia, Ananilea Nkya ameandika kupitia ukurasa wake wa X.
“Uchaguzi Mwenyekiti wa CHADEMA leo ndio utakaoamua endapo TZ itaendelea kuwa na upinzani DHAIFU au IMARA utakaoweza kuongoza wananchi kupigania MABADILIKO ya kweli bila woga au chuki ili kuinua maisha ya wananchi wote.Mjumbe kumbuka kura yako ndiyo itaamua,”
Edwin Odemba ameandika:
“Nawatakia uchaguzi mwema, amani upendo utamalaki miongoni mwenu, Nawatakia kila la kheri Mhe. Freeman Mbowe, Mhe. Odero C Odero, Mhe. Tundu Lissu.”
Dk Azaveli Lwaitama yeye ameandika kuitia ukurasa wake wa X akisema:
“Mungu wa kweli na mwema, tunaweka uchaguzi huu mikononi mwako. Tunaamini kuwa kwa uongozi wako, matokeo yatakuwa ya kutangaza utukufu wako na kuimarisha mshikamano wetu.”