
Mwanaharakati wa Haki za Binadamu wa nchini Tanzania, Maria Sarungi Tsehai, amehojiwa na kituo cha Televisheni cha NTV, Kenya, na kuelezea namna alivyotekwa na watu wasiojulikana.
Taarifa za Maria kutekwa zilisambaa kuanzia jana Jumapili, Januari 12, ambapo baadaye jioni Maria alijitokeza na kusema watekaji wamemuachia na yupo salama.
“Nipo salama nitazungumza kesho”alisema
Katika mahojiano na kituo hicho leo, Maria, amesema, watu waliomteka walikuwa wanne, watatu ndio walioshuka kwenye gari baada ya kumteka na walikuwa wakizunguka zunguka.
“Kulikuwa na dereva, mara ya mwisho kabla hawajaniachia, dereva pia alishuka, nikabaki na mtu wa kulia kwangu, aliyekuwa amenikaba amenishikilia, hakushuka nje ya gari muda wote, nadhani alikuwa ndiye alipewa jukumu la kunilinda,”amesema
Maria ameeleza kuwa, mara baada ya dereva wa gari hilo kushuka, alitumia muda mrefu kabla ya kurudi kwenye gari.
“Nadhani labda walikuwa wakitafuta ushauri, kulikuwa na mtu aliyekuwa akizungumza Kiswahili, nahisi alikuwa akipokea maagizo na nilikuwa nahisi wanatumia lugha ya alama kuwasiliana ili nisiwaelewe,” amesema.

Maria amesema, anaiona nchi ya Kenya kuwa na umoja, mshikamano na utawala wa sheria, kuliko Tanzania.
“Baada ya tukio la jana, nadhani kwa wale waliowahi kutekwa wanaelewa, Kenya ni salama zaidi kuliko nchi nyingine, natamani Kenya na Wakenya waelewe, namna gani ambavyo nchi yao ina nafuu ukilinganisha na nyingine,”amesema na kuongeza:
“Ninaweza kusema jambo moja, kitu kinachonifanya nione kuwa salama Kenya kuliko kingine chochote, ni umoja wa wakenya. Unapoona watu wanakutetea na hawajui wewe ni nani, niliambiwa kwenye mitandao ya kijamii watu walikuwa wananiteteta,kama vile ni wa kwao, kingine kinachonifanya nijione salama zaidi Kenya ukilinganisha na Tanzania ni utawala wa sheria wa Kenya , kwa mambo yaliyotokea, najisikia mwenye bahati sana ukilinganiusha na wengine waliotekwa”