Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) kimewekeza kiasi cha zaidi ya Tsh 2 bilioni kwenye utoaji wa elimu kwa njia ya madarasa janja, yatakayowezesha wanafunzi kupata elimu kwa njia ya mtandao na walimu kufundisha kwa njia ya mtandao.
Hayo yameelezwa na Mkuu wa IAA, Profesa Eliamani Sedoyeka, alipokuwa katika kikao kazi na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari hapa nchini.
Profesa Sedoyeka amesema, mwelekeo wa chuo hicho kwa sasa ni wa kimataifa ambapo chuo kimejipanga kuwekeza nchi za Comoro na Sudan Kusini.
“Tunaposema tunakwenda nje ya nchi, au kujenga chuo nje ya nchi, hiyo ni sehemu ya mipango tu, lakini katika kuwekeza nje ya nchi kuna shauri za kitaalamu katika sekta binafsi na za serikali katika nchi tunazokwenda,kuna tafiti mbalimbali pia tunazoweza kufanya,” amesema
Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), Umoja wa mataifa umesisitiza umuhimu wa kutumia mapinduzi ya kidijitali ili kuongeza ufanisi katika elimu jumuishi.
Unesco katika ripoti hiyo, limeeleza kuwa, nchi wanachama wa UNESCO lazima wafanye mabadiliko ya sera za kitaifa ili kutumia teknolojia katika ufundishaji na ujifunzaji.
“Katika muktadha huu, elimu kwa njia ya teknolojia imekuwa sehemu muhimu katika mipango ya kitaifa kwa lengo la kukuza usawa na ubora katika elimu.” Imesema ripoti hiyo
Akizungumza na wahariri hao, Profesa Sedoyeka amesema, madarasa janja, au ‘smart classes’ yatawawezesha walimu kufundisha na wanafunzi kujifunza kwa kupitia teknolojia ya mawasiliano.
‘Madarasa sio lazima tuwapeleke walimu nje ya nchi, walimu wanaweza kufundisha wakiwa hapa, mihadhara ya kitaaluma itakuwa imerekodiwa milele na hivyo mwanafunzi anaweza kucheza video ile na kufanya marejeo wakati wowote,” amesema Profesa Sedoyeka na kuongeza:
“Lengo letu ni kuwezesha ujifunzaji, kuleta tija ya ufundishaji na tija katika marejeo.”
Uwekezaji huu katika TEHAMA, unafanywa chini ya Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) uliofadhiliwa na Benki ya Dunia(WB) ambapo kiasi cha Tsh 1.4 bilioni kimetengwa na fedha nyingine katika uwekezaji huu ni mapato ya ndani, kiasi cha Tsh 1.4 bilioni.