Saa chache baada ya Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana wa ACT-Wazalendo, Abdul Nondo kutekwa na kisha kutupwa eneo la Coco Beach na gari linalodhaniwa kuwa la Polisi, chama hicho kimelihoji maswali manne jeshi la polisi Tanzania .
Naibu Katibu Mkuu wa ngome ya Vijana wa ACT- Wazalendo, Rukaiya Nassir ametoa taarifa kwa umma akihoji, maswali baada ya Nondo kupatikana.
MASWALI YA ACT-Wazalendo yalikuwa haya:
- Je wamebaini zile pingu ambazo tunajua haziuzwi kama njugu au karanga zilizoanguka na kuokotwa zilikuwa za nani?
- Je wamechukua hatua gani kuhusu taarifa za awali kuhusu Deogratius Minja, mmiliki wa gari lililotumika kumteka Mwenyekiti wetu.
- Je wamechukua hatua gani dhidi ya polisi wa kituo cha Gogoni ambapp gari lililotumika kumteka Mwenyekiti wetu kuwepo pale?
- Je wamebaini polisi waliohusika kumteka, kumpiga na kumtelekeza Mwenyekiti wetu?
Taarifa za kutekwa kwa Nondo ziliripotiwa na msamaria mwema aliyempigia Katibu Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika na kumweleza kuwa gari limeonekana likimchukua kwa nguvu Nondo eneo la stendi ya Mbezi, Magufuli.
Jeshi la Polisi, kupitia taarifa yake iliyosainiwa na Msemaji wa Jeshi hilo, David Misime imeeleza kuwa polisi wanafanya uchunguzi kuhusu tukio hilo.