Dar es Salaam. Wakati bado jitihada za kuwaokoa walionasa kwenye kifusi baada ya jengo la ghorofa kuporomoka, Ilala Kariakoo, Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Profesa Mohamed Janabi amesema wamewapitishia walioanaswa, kifaa cha kupima wingi wa hewa ya oksijeni.
Profesa Janabi ameyasema hayo jana na kusema kuwa wameingiza vifaa vidogo, vinavyofahamika kitaalamu kama oksijeni ‘oximiter’ ili kujua iwapo hewa waliyonayo huko chini inawatosha.
“Tunataka asilimia ya hewa iwe 90, ikiwa chini ya 90 itatufahamisha kuna haja ya kuongeza oksijeni” amesema na kuongeza:“Sisi zaidi tupo pale kwa ajili ya tiba”
Amesema majeruhi wanaookolewa hupatiwa huduma ya kwanza na baadaye kupelekwa hospitali lakini kikubwa wanachofanya na kuhakikisha wataalamu wa afya wanawapiga ‘ultrasound’ wote walionusurika ili kujua iwapo kuna majeraha ya ndani kwa ndani.
Zoezi la uokoaji limeingia siku ya tano leo baada ya jengo hilo la ghorofa kuporomoka Novemba 16. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameshauri kuongezwa muda wa zoezi la uokoaji.
Mpaka sasa waliothibitishwa kufariki dunia ni 16 na majeruhi ni 87.