Wino Ripota
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amesema, licha ya utaratibu wa uokoaji katika majanga ya kidunia kuelekeza kuwa muda wa saa 72 kutumika katika zoezi la uokoaji, ameshauri kuongezwe saa 24.
Ameyasema hayo kupitia mtandao wa X, ambao amekuwa akiutumia zaidi kuwasiliana na kusema amezungumza kwa kirefu na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, kuhusu maendeleo ya zoezi hilo la uoakaji na kushauri saa 24 ziongezwe.
“Licha ya utaratibu huo, binafsi nina matumaini kuwa Mwenyezi Mungu huweka mkono wake katika changamoto za aina hii, na hivyo basi nimemuelekeza kuongeza saa 24 zaidi kwenye zoezi hili, ili kuendelea kuwapambania ndugu zetu ambao tunaamini bado wako hai”
Rais ameyasema hayo ikiwa ni siku mbili chache baada ya jengo la ghorofa eneo la Kariakoo, wilaya ya Ilala, jijini hapa kuporomoka.
Hadi sasa watu 16 wamethibitishwa kupoteza maisha na wengine 86 wameokolewa na wanaendelea na matibabu.
Rais amesema baada ya saa 24 hizo kumalizika ifanyike tena tathmini ya kina kabla ya maamuzi yoyote juu ya mwelekeo wa zoezi hilo.
“Maisha na uhai wa kila binadamu ni zawadi ya kipekee toka kwa Mwenyezi Mungu na kama Taifa, uhai na maisha ya Mtanzania yeyote ni lazima kupiganiwa kwa hali na nguvu zote. Tuendelee kuwaombea ndugu zetu ambao bado wamekwama kwenye ajali hii.” Amesema