Dar es Salaam. Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imetoa taarifa ikionyesha kupokea maombi ya leseni kutoka kwa kampuni ya Sterlink, inayomilikiwa na mtu Tajiri zaidi duniani, Elon Musk, ikiomba kibali cha kusambaza intaneti yenye kasi.
Mamlaka hiyo imetoa siku 14 kwa yeyote mwenye ‘neno’ kuhusu ombi hilo la Starlink kutaka kuwekeza katika biashara ya intaneti hapa nchini.
Awali, Musk aliwahi kunukuliwa akisema, kampuni yake imeshindwa kuanza kazi, Tanzania kwa sababu ya changamoto za kupata kibali kamili.
Lakini leo, Novemba 15 TCRA, imetoa siku 14 kabla ya kutoa maamuzi kamili ya kuipa kibali Sterlink.
Starlink ambayo inamilikiwa na kampuni ya SpaceX ilianza kuingia katika soko la Afrika Mashariki, mwaka jana, ambapo mpaka sasa tayari nchi za Kenya na Rwanda zimeshaanza kunufaika na intaneti yenye spidi kali.
Lakini wataalamu wa mawasiliano hapa nchini wamesema wanachotarajia iwapo Starlink itaanza kazi.
Mwanahabari mkongwe na Mjumbe wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) Neville Meena amesema ujio wa kampuni ya Sterlink, utaleta mapinduzi makubwa katika sekta ya mawasiliano nchini.
“Yale masuala ya udukuzi sasa hatutayatarajia kwa sababu hii intaneti ya Musk, inatumia satelaiti, lakini kasi ya intaneti itarahisisha zaidi kazi za kihabari, na kuwasaidia zaidi wanahabari na wapashaji wa habari” amesema
Mtaalamu mawasiliano na intaneti, Jackson Peter, amesema ni muhimu kwa Starlink kuruhusiwa ili kuwe na ushindani kwani kwa sasa kampuni za simu zilizopo zinatoa huduma za intaneti kwa bei ya juu na huduma zisizo na uhakika.
Henry Mwakajumba, mtumiaji wa mitandao ya kijamii amesema:
“Ushindani unaleta huduma bora kwa jamii na kupunguza kero za intaneti kwenye nchi yetu”
Juhudi za Starlink kuanzisha huduma hapa nchini zimekuwa zikikwama kutokana na mazungumzo marefu baina yake na serikali ya Tanzania.
Masuala hayo ni yale yanayohusiana na ugawaji wa haki za wigo, ambayo ni muhimu kwa ajili ya uendeshaji wa huduma za mtandao wa satelaiti.
Kadhalika Starlink inalazimika kuhakikisha kuwa huduma zake zinazingatia kanuni za ulinzi na faragha za Tanzania.
Musk ndiye mmiliki wa sasa wa mtandao wa X, zamani Twitter.