Wino Ripota
Taasisi ya Kimataifa ya kuboresha elimu kwa Watoto wa kike (CAMFED) imeshauri kuwepo kwa sheria kamili itakayoruhusu Watoto wa kike wanaopata ujauzito wakiwa shuleni, kurejea katika mfumo rasmi wa elimu.
Akizungumza leo katika kongamano la kimataifa la kuboresha elimu(IQEC), Mkurugenzi wa Miradi na Ushirikiano wa CAMFED-Tanzania Ana Sawaki amesema matamanio ya wadau wa elimu ni kuona kuna mfumo jumuishi wa elimu kisheria, ambao unatoa elimu kwa Watoto wote bila kujali hali zao.
Sawaki, amesema wasiwasi uliopo ni iwapo kiongozi mwingine wa Tanzania atakuwa na utashi kama alionao Rais wa sasa wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.
“Baada ya mama kuchaguliwa ameruhusu hata watoto ambao walipata ujauzito na walifukuzwa shule kwa sababu mbalimbali wamerudi shule, ni kitu kizuri,lakini sasa kiko kwenye mfumo? ama ni utashi, kwamba ikitokea kwamba mama amemaliza muda wake, akija mwingine atakuwa na utashi unaofanana, Hapana, inawezekana ikawa tofauti,” amesema Sawaki.
Rais Samia Suluhu aliondoa zuio lililowekwa na mtangulizi wake, Hayati John Magufuli, la kuwazuia Watoto wa kike waliopata ujauzito kuendelea na elimu.
Sawaki amesema, ni vyema kukiwa na mifumo na sera ambazo ni jumuishi bila kuangalia hali zao za ulemavu, umaskini, mazingira ya kijiografia au maeneo wanakotoka.
Kwa mujibu wa Sawaki, CAMFED inalenga kuwasaidia Watoto wa kike Tanzania kupata elimu, ambapo mpaka sasa, Watoto zaidi ya 590,000 wamesaidiwa kupata elimu na vifaa vya elimu kwa ngazi ya sekondari.
“Tumekuwa tukiwasaidia Watoto kupata viatu, madaftari, nafasi za bweni, taulo za kike na kwa ngazi za Diploma na Chuo Kikuu, wasichana wapatao 5600 wamesaidiwa mpaka sasa.” Amesema
Sawaki amesema changamoto wanayoiona ni uhitaji wa watoto wanaotoka katika mazingira magumu na akasema mashirika yasiyo ya kiserikali na hata ya kiserikali hayawezi kutatua changamoto hiyo peke yake.
Kwa upande wao, Mtandao wa Elimu Tanzania, (TenMet) ambao ni waandaji wa kongamano hilo, wamesema linalenga kuangalia fursa na changamogto zilizopo katika mifumo bora na thabiti ya elimu zaidi ya darasani.
Mratibu wa TenMet Tanzania, Martha Makala amesema lengo la kongamano hili ni kuangalia namna bora ya kuimarisha elimu na huku akisisitiza elimu endelevu kwa watu wote, bila ukomo.
Amesema mjadala utakaotawala kwa siku ya kesho na alhamisi, ni namna ya kuimarisha elimu Tanzania na kujadili elimu endelevu kwa njia ya teknolojia.
“Tunataka kuwa na mifumo imara inayoweza kutoa elimu zaidi ya darasani, lakini pia kipindi cha majanga, mvua, tetemeko la ardhi, je wanafunzi wetu wataendelea kusoma kama kawaida,” amesema Makala.
Kongamano hilo limeshirikisha wadau zaidi ya 300 kutoka mataifa mbalimbali Afrika na litafanyika kwa siku tatu hapa jijini Dar es Salaam.
Hongereni sana CAMFED kwa kuliona hili, ni kweli Mama akiondoka, inawezakana Rais mwingine akaturudisha tulipotoka. Ni muhimu mabadiliko haya yawekwe kwenye sheria ya nchi.
Asante kwa kuwasiliana na Wino Tanzania, Karibu sana.