
Wino Ripota
Aghalabu unapozikuta kondomu katika vituo vya afya, maduka ya dawa, hoteli au nyumba za wageni, wazo lako litakwenda katika matumizi ya kifaa hicho ambayo kimsingi ni tendo la ndoa.
Hata hivyo, imebainika kuwa kondomu, badala ya kutumiwa kama zana ya kujikinga na maambukizi ya magonjwa ya zinaa hasa UKIMWI, hivi sasa inatumika kama nyenzo ya kuwafukuza tembo wanaovamia makazi ya watu katika maeneo yaliyo karibu na hifadhi hapa nchini.
Ni katika wilaya ya Katavi, Kijiji chaMwese, Tanganyika, ameketi Mwina Masambo, akiwa amejishika shavu kwa mkono wake wa kulia, Mwina anaeleza jinsi alivyompoteza mume wake, Daniel Masambo, kwa kushambuliwa na tembo.
“Tembo wanafika mara nyingi katika makazi ya watu, wanaingia mashambani kutafuta vyakula sasa, imekuwa ni kama vita kati yetu, mkimuwahi inakuwa bahati yenu, akiwawahi, mnakufa,” anasema Mina
Mume wa Mina amefariki, mwaka 2019, akiwa shambani kwake, mita chache kutoka yalipo makazi yao.
“Siku hiyo alikwenda kufanya kazi zake za shambani kama kawaida, lakini baada ya muda tukasikia kelele nyingi, tulipokimbilia, tukakuta tayari tembo amemkanyaga. Hatukuwahi hata Kwenda hospitali akafariki,” anasema Mina.
Vita hii kati ya wanyamapori hasa tembo na wakazi inaongezeka kwa sababu, tafiti zinaonyesha kuwa tembo wanatafuta chakula, maji na wanapenda ukimya. Hivyo wanapofika kwenye makazi ya watu wanakerwa na kelele zao.
Tembo hula kiasi cha kilo 400 za chakula kwa siku, hivyo inaelezwa, kuvamia kwao makazi ni katika harakati za kusaka mlo wao.
Ili kukabiliana na uvamizi wa wanyama, wakazi wa maeneo yenye wanyama kama tembo wamebuni mbinu ya kuwakabili bila kuleta madhara makubwa.
Algert Mdoe, mkazi wa Katavi anasema ili kukabiliana na Wanyama hasa tembo, wanatumia mipira ya kiume, kondomu, na kuiweka pilipili iliyosagwa na kisha huwarushia tembo pindi wanapovamia makazi.
“Tembo kwa kawaida wanaogopa pilipili, kwa hiyo hili linakuwa ni kama bomu la mkono, tukilirusha, tembo hafiki maeneo haya,” anasema
CONDOM NA PILIPILI VINATUMIKAJE KUFUKUZA TEMBO?
Taasisi ya utunzaji wa mazingira, Nature Conservancy, inawapa mafunzo maofisa wanyamapori na wadau wa mazingira Tanzania, kutumia mbinu hii isiyo na gharama na isiyo na madhara kwa Wanyama kama tembo wanaovamia makazi, kuharibu mazao na kuua.
“Unachukua mpira wa kiume (condom) unachanganya pilipili na unga, udongo kiasi ili kuweka uzito kwenye condom, kisha unapoona tembo, unawarushia tembo,” anasema
Kwa mujibu wa ‘Nature Conservancy,’ tembo wanaogopa pilipili kwa sababu ikiwangia masikioni na puani huwasababishia muwasho unaowakera.
“Hii njia ni rahisi na isiyoweza kuleta madhara kama kifo na kwa tembo,” anasema Mdoe
Juma Massay, mkazi wa Katavi, anasema awali wakazi walikuwa wanawawinda tembo kwa kutumia silaha kama mikuki na gobore, lakini hilo lilisababisha Wanyama hao ambao ni kvutio cha utalii kupungua.
“Sasa njia nyingine tuliyojifunza ni kufuga nyuki mashambani, kwa sababu tembo wanaogopa sana nyuki.” Anasema Massay.
Takwimu za Mamlaka ya wanyamapori Tanzania (TAWA) zinaonyesha kuwa, matukio ya Wanyama kuingia kwenye makazi ya watu Tanzania yaliongezeka kutoka 833 mwaka 2016/17 hadi kufikia 997, na mwaka 2018/19 matukio hayo yalifikia 2817.
Nchi zenye wingi wa tembo ndizo zenye changamoto zaidi, kwa mfano Zimbabwe, ina tembo 100,000. Tanzania ina idadi ya tembo 60,000 na Kenya wana tembo 35,000.
Tafiti zinaonyesha zaidi kuwa migogoro kati ya Wanyama na wanakijiji wanaoishi karibu na hifadhi, inaongezeka kila siku.