Wakati Jeshi la Polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam, likitangaza kumshikilia mkazi wa Salasala Derick Junior, kwa tuhuma za kumjeruhi na kumtishia kwa bostola, Julian Bujuru, Wakili Peter Kibatala ametangaza yuko tayari kumsaidia. Kwa sasa Bujuru amelazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), akiendelea kupatiwa matibabu.
Tukio hilo lilitokea jana Oktoba 27, 2024 saa 12 asubuhi maeneo ya Masaki kwenye jengo lenye klabu ya ‘1245 night club’ ambapo, Derick alimjeruhi Bujuru kwa kumpiga na kitako cha bastola na sehemu mbalimbali na kumjeruhi.
Hata hivyo, uongozi wa 1245 night club, umetoa taarifa kwa umma vurugu hizo zilizotokea ghorofa ya chini ya jengo ambalo klabu hiyo ya usiku inapatikana.
“Tunapenda kufafanua kwamba 1245 iko kwenye ghorofa ya nne, na tukio hili lilitokea nje ya maeneo ya karibu ya maeneo ya kupumzika na mgahawa.
“Tunalaani vitendo vyote vya vurugu vinavyopingana na dhamira yetu ya kutoa huduma bora katika mazingira salama,” ilieleza taarifa hiyo.
Na kuongeza kuwa uongozi wa 1245 una sera zinazokataza mtu kuingia na silaha za moto katika eneo hilo, kwa kuwa ulinzi na usalama kwa wateja ndio kipaumbele hivyo, wapo tayari kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi.
Kabla ya Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam, Jumanne Muliro kuzungumza wanahabari mtandaoni kulisambaa video ya picha mjongefu zilizorekodiwa na CCTV Camera zikimuonyesha Derick akimshambulia Bujuru.
Katika tukio hilo, lililorekodiwa kwenye korido pembezoni mwa lifti za jengo hilo, Junior alionekana akiwa na bastola na kumjeruhi Bujuru kwa kitako cha silaha hiyo, sambamba na kumpiga mtama huku wakionekana wanawake wawili wakijaribu kumtuliza.
“Kufuatia tukio hilo Jeshi la Polisi linaendelea kutoa onyo na tahadhari kwa wote wanaomiliki silaha kihalali kwamba, halitavumilia kuona wakizitumia kinyume cha sheria, kanuni na miongozo waliopata kuhusu umiliki wa silaha.
“Polisi baada ya kufuatilia limebaini mtuhumiwa huyu aliomba silaha kwa utaratibu unaotakiwa, lakini kulingana na jeshi limekamilisha uchunguzi wake na linapeleka mashtaka kwenye Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kwa hatua za kisheria zaidi,” amesema Muliro.
Kutokana na hilo, Kamanda Muliro amesema jeshi la polisi linaandika taarifa kwenye mamlaka zilizopo ndani ya jeshi hilo, ili kuhakikisha mtuhumiwa ananyang’anywa silaha kisheria kama alivyokabidhiwa wakati wa kuomba.
“Hatutavumilia mtu yeyote anayemiliki silaha kukiuka masharti na taratibu za umiliki huo, ukikiuka hatua kali zitachukuliwa,” amesema Muliro.
Katika hatua nyingine, wakili Kibatala amejitosa katika sakata hilo, akimtaka Bujuru kuwasiliana naye kwa ajili ya kutoa msaada wa kisheria kwa changamoto iliyomkumba.
Katika akaunti yake ya Instagram Kibatala aliweka picha ya video hiyo na kuandika: “Mpendwa mwathirika wa tukio hili, samahani naomba tuwasiliane. Tafadhali wasiliana na mimi tuanze kuchukua hatua,” amesema Kibatala