Wino Tanzania
Saa chache baada ya kusambaa kwa picha mjongeo inayomuonyesha mtu mmoja, aliyetajwa kwa jina la Derick Juniori, akimshambulia kwa silaha mwanaume ambaye jina lake halikufahamika mara moja kwa kitako cha bastola, Jeshi la polisi limesema tayari limemkamata mtu huyo.
Picha hizo mjongeo zilisambaa kwenye mitandao ya kijamii kuanzia usiku wa kuamkia leo, Oktoba 28, ambapo zilionyesha wanaume hao wawili wakiwa sambamba na wanawake wawili, na kisha mwanaume mmoja aliyekuwa amevalia shati jeupe alionekana akimshambulia kwa kutumia kitako cha bastola, mwanaume mwingine aliyekuwa na shati lenye rangi nyeusi.
Kwa mujibu wa Jeshi la Polisi, tukio hilo limetoka usiku wa saa 6:30 eneo la Masaki, wilaya ya Kinondoni, katika Klabu iliyotajwa kwa jina la 1245, ambapo mtuhumiwa, aliyetajwa kwa jina la Derick Derick Junior, alimjeruhi, Julian Bujuru.
“Mtuhumiwa alimjeruhi Julian Bujuru kwa kumpiga na kitako cha bastola na pia kumjeruhi sehemu ya jicho na pua” imesema taarifa hiyo ya jeshi la polisi, iliyosainiwa na Kamanda wa Kanda Maalum ya Polisi, Mkoa wa Dar es Salaam,SACP, Muliro .J. Muliro.