Zamani tuliamini katika kiapo cha ndoa, kisemacho: Hadi kifo kitutenganishe, lakini uhaba wa nafasi za kuzikia, ubora na umaarufu wa maeneo ya kuzikia, umesababisha baadhi ya wanandoa waliokufa kwa nyakati tofauti sasa kuzikwa katika kaburi moja. Kwa maana hiyo, tunaweza kusema, kifo kimewakutanisha tena.
Wino-Tanzania, imefanya utafiti wa kina katika maeneo maarufu ya kuzikia jijini Dar es Salaam, Kinondoni, Kisutu, Sinza na Temeke.
Katika makaburi ya Kinondoni, WINO-Tanzania imebaini kuwa kutokana na nafasi finyu za kuzikia, wakati huo watanzania wengi wakipenda kuzikwa katika makaburi hayo maarufu, uongozi wa manispaa umeruhusu huduma ya kuzika miili, miwili miwili, iwapo ni wanandoa au ndugu.
Nasibu Limira, msimamizi wa makaburi ya Kinondoni, amesema, ili kupata kibali cha kuzika watu wawili katika kaburi moja, basi wanafamilia wanatakiwa kupata kibali kutoka ofisi yake lakini ni baada ya wanafamilia hao kukubaliana pia.
Tazama na ona zaidi habari hii kwa https://www.instagram.com/p/C_Sa6d8odzo
Hata hivyokwa mujibu wa msimamizi wa makaburi ya Kinondoni, Nasibu kwa sasa makaburi hayo yamejaa na manispaa ya Kinondoni, imetenga eneo jingine la Kwa Kondo kwa ajili ya kuzikia.
“Makaburi ya Kinondoni, yamesitisha kuzika katika eneo hilo tangu mwaka 2015, na sasa watu wanazikwa eneo la Kwa Kondo, Ununio.
Makaburi ya Kinondoni ni miongoni mwa maeneo kongwe ya kuzikia hapa Tanzania, yaliyoanzishwa miaka ya 1930.
Wino imeshuhudia makaburi ya watu mashuhuri katika eneo hili akiwamo Muigizaji wa filamu, Steven Kanumba, aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu, Amatus Liyumba, Msanii, Adam Kuambiana, Mawaziri kadhaa na aliyekuwa mtangazaji wa Clouds Ephrahim Kibonde.
Inaelezwa kuwa pengine ndicho chanzo cha wengi kupenda kuzika wapendwa wao eneo hili.